Kampuni ‘hewa’ ilivyopewa tenda kutengeneza meli tano Tanzania

0
36

Rais Samia Suluhu Hassan amezivunja Bodi za Wakurugenzi wa Shirika la Bandari Tanzania (TPA) na Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kutokana na tuhuma za mwenendo usio sawa kwenye mkataba wa zaidi ya TZS bilioni 400 kujenga meli tano kati ya TPA na kampuni ya YÜTEK ya nchini Uturuki.

Rais amechukua hatua hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa matumizi ya Mradi wa Maboresho ya Miundombinu ya Gati namba 0 hadi 7 pamoja na uongezaji wa kina cha bahari katika lango kuu la bandari katika hafla iliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema kwamba baada ya kutilia mashaka kampuni hiyo aliunda timu ambayo ilikwenda Uturuki kufuatilia kampuni ndipo walipobaini kwamba haitambuliki miongoni mwa kampuni zinazotengeneza meli, haina ofisi na haina uwezo wa kifedha na kitaalamu.

Ameeleza kwamba inachofanya kampuni hiyo ni kuchukua tenda na kutafuta kampuni zenye uwezo kufanya kazi hiyo. Hata hivyo ameeleza kushangazwa na mamlaka za bandari kusema kwamba zilifanya uchunguzi na kujiridhisha na uwezo kampuni hiyo.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam amesema licha ya mwenendo kuonesha kuwa mapato yanayongezeka, bado yanaweza kuongezeka zaidi endapo hatua madhubuti zingechukuliwa kudhibiti upotevu.

Ripoti maalum imeonesha upotevu wa fedha nyingi zilizotumika kuajiri Makampuni mbalimbali ya kuanzisha mifumo ya kielekroniki ya ukusanyaji wa mapato ambayo haikutoa tija iliyokusudiwa.

Amezitaja Kampuni hizo kuwa ni Soft Tech Consultant Ltd ambayo ilipewa zabuni ya shilingi milioni 694 na kulipwa shilingi milioni 600, Kampuni ya Twenty Third Centuary System ilipewa kazi ya Dola za Marekani milioni 6.6 na kulipwa Dola milioni 4.6 na mkataba kuvunjwa na Kampuni ya SAP – East Africa Ltd iliyopewa Dola za Marekani 433,000 Mshauri Mwelekezi binafsi alilipwa Dola za Marekani 31,920.

Amemuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kupitia ripoti hiyo na kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika.

Send this to a friend