Kampuni iliyokuwa imekataa kuongeza thamani ya madini nchini yasalimu amri

0
40

Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Madini isimamie kikamilifu suala la uongezaji thamani ya madini nchini na kubainisha kuwa uchenjuaji wa madini utafanyika Tanzania na sio nchi nyingine.

Amesisitiza kuwa madini yetu yatachimbwa, kuchenjuliwa na kuongezwa thamani hapa nchini ili kuweza kupata faida tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.

Amesema hayo katika hafla ya Uwekaji Saini Makubaliano kati ya Serikali na kampuni 4 za uchimbaji madini, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza alisema kuwa kampuni hizo zilitakiwa kuwa tano, lakini awali moja ilikataa utaratibu wa kuongeza thamani ya madini nchini, lakini majadiliano yaliendelea, na baada ya kuona msimamo wa serikali wakakubali.

Kufuatia uamuzi huo, Rais ameiagiza Wizara ya Madini kusaini makubaliano na kampuni hiyo ambayo nayo itafanya shughuli zote za madini hapa nchini.

Kampuni hizo zinatarajiwa kuwekeza shilingi Trilioni 1.75, ambapo miradi hiyo pamoja na kuipatia mapato Serikali pia itatoa fursa za ajira, gawio na biashara kupitia huduma zitakazotolewa katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na usafirishaji wa madini yatakayozalishwa.

Rais Samia amesema kupitia miradi hiyo, Serikali itapata manufaa mbalimbali ikiwemo kodi, tozo, ajira, huduma kwa jamii, ununuzi wa bidhaa na huduma zinazopatikana hapa nchini.

Amewataka wawekezaji kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia sekta hiyo na kuagiza araza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Serikali za Mitaa pamoja na wawekezaji kusimamia utunzwaji wa mazingira kama Sheria ya Mazingira inavyobainisha na kuhakikisha kuwa miradi hiyo haileti athari katika maeneo mbalimbali.

Send this to a friend