Kampuni ya Australia iliyofutiwa leseni yatishia kukamata ndege ya Tanzania

0
43

Kampuni ya Indiana Resources ya Australia imetishia kuikamata ndege ya Tanzania endapo itashindwa kulipa fidia kufuatia kesi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Uwekezaji (ICSID) nchini Marekani.

Kampuni hiyo imeishitaki Tanzania baada ya kutaifisha leseni ya uchimbaji madini katika mradi wa Ntaka Hill Nickel bila fidia yoyote wakati wa uongozi wa Hayati Dkt. John Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bronwyn Barnes ameiambia The African Report kuwa hatosita kuishikilia ndege ya Tanzania endapo itashindwa kulipa fidia kama itakavyoamuliwa na ICSID.

“Tanzania ilichukua mali yangu. Nami nina furaha kufanya vivyo hivyo,” amesema.

ATCL yatangaza mabadiliko ya ratiba kutokana na uchache wa ndege

Barnes amesema shitaka hilo lina thamani ya takribani TZS bilioni 234.5, na Indiana inastahili kupata asilimia 60 ya fedha hiyo, kiasi ambacho amesema kuwa hata thamani ya ndege haitoshelezi.

Licha ya kuwa uamuzi wa mgogoro huo haujatolewa uamuzi, Barnes amesema anaamini watashinda kwa sababu kuna kila sababu ya wao kustahili kulipwa fidia.

Wakati hayo yakiendelea ndege ya Tanzania inaendelea kushikiliwa nchini Uholanzi tangu Desemba 2022 na kampuni ya Sweden kushinda tuzo ya TZS bilioni 380 dhidi ya Tanzania. Hata hivyo Tanzania ilisema kuwa imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

Jitihada za kuwapata Wakala wa Ndege za Serikali kuhusu taarifa hiyo hazikufanikiwa.

Send this to a friend