Kampuni ya Barrick yachangia mapato ya TZS trilioni 3.6 serikalini kwa miaka minne

0
10

Kampuni ya uchimbaji madini ya Dhahabu ya Barrick imechangia kiasi cha shilingi trilioni 3.6 katika mapato ya serikali kupitia kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Meneja Mkaazi wa kampuni hiyo nchini Dkt. Melkiory Ngido mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akiwasilisha maendeleo ya kampuni tanzu baina ya Barrick Gold na serikali ya Tanzania inayofahamika kama Twiga Minerals.

Dkt. Ngido ameelezea kuwa, kwa mujibu wa takwimu za miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, kampuni ya Barrick imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 4.24 [TZS trilioni 11] katika shughuli zake ndani ya nchi, huku dola za Marekani bilioni 1.5 [sawa na TZS trilioni 3.6] zikilipwa serikalini kupitia kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali.

Amesema kampuni ya Barrick ilipochukua usimamizi wa shughuli zake nchini Tanzania mnano mwaka 2019, imeendelea kuwa mdau mkubwa wa uchumi kupitia uwekezaji, ajira, na miradi ya kijamii.

Akizungumzia mchango wa kiuchumi, Dkt. Ngido ameelezea kuwa kiasi cha dola za Marekani milioni 158 [sawa na TZS bilioni 412.4], hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 4 zimelipwa kama gawio la serikali kutokana na ubia huo.

Sambamba na hilo, amesema kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.3 [TZS trilioni 6.04], hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 55 ya matumizi yote yameelekezwa kwa wasambazaji wa ndani, huku asilimia 32 ya uwekezaji huo, ukihusisha kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.37 imelipwa kama kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali kwa serikali.

Ameongeza kuwa kiasi cha dola milini 397 milioni [TZS trilioni 1.03] sawa na asilimia 9 zimetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi huku dola milioni 30 [TZS bilioni 78.3] zikitumika kwenye utafiti wa madini katika maeneo hayo na kiasi cha dola milioni 15.6 sawa na shilingi bilioni 40.7 zimeelekezwa kwenye miradi ya kijamii.

Kuhusu suala la ajira kwa Watanzania, Dkt. Ngido amesisitiza kuwa Barrick imejizatiti katika kutoa ajira kwa Watanzania, ambapo asilimia 96 ya wafanyakazi wake ni raia wa Tanzania, na kwa sasa kampuni hiyo ina wafanyakazi 6,185 kati yao 5,933 ni Watanzania, huku wageni wakiwa asilimia 4 pekee, na kwamba asilimia 53 ya wafanyakazi hao wametoka kwenye jamii zinazozunguka migodi.

Ameongeza kuwa, asilimia 100 ya nafasi za juu za usimamizi zinashikiliwa na Watanzania huku uwakilishi wa wanawake ukiwa ni asilimia 13 ya wafanyakazi wote.

Ikumbukwe kuwa, Ripoti ya 14 ya Taasisi ya Uhamasishaji uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi asilia (TEITI) iliyochapishwa mwezi Juni 2024 imethibitisha kuwa kampuni ya Barrick Tanzania imechangia asilimia 51 ya mapato ya serikali, yote yaliyotokana na tasnia ya uziduaji, ikiwa ni mchangiaji mkubwa kama taasisi moja katika uchumi.

Send this to a friend