Kampuni ya kubeti yaamriwa kumlipa John Bocco TZS milioni 200

0
53

Mahakama Kuu ya Tanzania imeiamuru kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Princes Leisure (T) Ltd ya jijini Dar es Salaam kumlipa mchezaji wa Simba, John Bocco shilingi milioni 200 kwa kutumia picha yake katika tangazo la biashara  bila ruhusa yake.

Tangazo hilo lililochapishwa likiwa na picha ya Bocco lilitolewa kati ya Novemba 18 hadi Desemba 1, 2021 katika ukurasa wa Instagram wa kampuni hiyo likiwa na ujumbe ulisomeka; “Uhondo wa Ligi NBC unaendelea leo kwa mechi 3. Kubwa zaidi ni Simba watakuwa wageni wa Ruvu Shooting huko Mwanza kwenye dimba la CCM Kirumba. Siku za Pesa zimerejea.”

Katika kesi hiyo ambayo Bocco aliwakilishwa na mawakili Innocent Michael na Gadi Kabele, amesema kutumiwa kwa picha yake kulimaanisha amevunja mkataba wake na Simba ambayo ilikuwa mbioni kumchukulia hatua za kinidhamu, hivyo aliomba mahakama iiamuru kampuni hiyo kumlipa TZS bilioni 1 kama fidia, na kumlipa mrabaha wa asilimia 25 kwa kipindi chote ilichoitumia.

Kesi hiyo ambayo imetolewa hukumu Agosti 31, mwaka huu imesikilizwa chini ya Jaji Irvin Mugeta kwa upande mmoja (ex parte) kwa kuwa mdaiwa aliondolewa katika mwenendo wa shauri hilo baada ya kushindwa kuwasilisha utetezi wake kwa maandishi katika muda ulio ndani ya sheria.

Send this to a friend