Stockholm, Sweden: Kampuni ya Scania imeipongeza Tanzania kwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira, na kwamba wanavutiwa mabadiliko mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania ikiwemo uboreshaji wa sekta ya uwekezaji.
Hayo yamesemwa na mkuu wa teknolojia endelevu ya usafirishaji wa Kampuni ya Scania, Fredrik Wijkander wakati akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, na kuongeza kuwa maboresho hayo yanawapa hamasa ya kushirikiana na Tanzania katika sekta ya usafirishaji hususani usafiri wa mizigo na abiria.
Dkt. Mpango ambaye yuko nchini humo kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 ametembelea makao makuu ya kampuni hiyo na kushuhudia teknolojia ya utengenezaji wa magari yanayotumia nishati ya gesi, ikiwemo gesi inayotokana na taka ngumu, ili kupunguza ongezeko la gesi joto duniani.
Ameiambia kampuni hiyo kuwa Tanzania ipo tayari kwa ajili ya ushirikiano hasa katika vyuo vya ufundi vitakavyowezesha uhamilishaji wa teknolojia.
Aidha, ameikaribisha kampuni hiyo kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji wa sekta ya usafiri waliopo Tanzania ili kueneza teknolojia ya matumizi ya nishati mbadala katika usafirishaji na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.