Kampuni ya Total yasitisha ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda-Tanzania

0
41

Kampuni ya mafuta ya Total imesitisha mpango ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania, baada ya kushindwa kununua sehemu ya mradi wa mafuta unaomilikiwa na Kampuni ya Tullow Oil Plc nchini Uganda.

Total kutoka nchini Ufaransa imesitisha shughuli zote zilizokuwa zinahusiana na mradi huo wenye thamani ya TZS trilioni 8 ambao una urefu wa kilomita 1,445, kwa sababu umiliki wenza (shared ownership) ulikuwa uamuliwe baada ya kukamilia kwa dili la kununua sehemu ya mradi wa Tullow.

Wiki iliyopita Tullow ililazimika kusitisha mpango wa kuuza sehemu ya mradi wake kwa kampuni ya Total ya Ufaransa na Cnooc Uganda Ltd ya China, na kuanza upya mchakato wa uuzaji kutokana na masuala ya kodi kukwamisha uuzaji huo. Kuvunjika kwa makubaliano hayo kumekuwa ni hasara kwa Tullow ambayo ilitarajia washirika hao wangeisaidia kuzalisha mapipa bilioni 1.5 ya mafuta katika mradi wake wa Uganda.

Baada ya Tullow kugundua mafuta nchini Uganda mwaka 2006, nchi hiyo iliweka lengo la kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta na bomba litakaloweza kusafirisha mafuta mapipa 216,000 kwa siku, malengo ambayo yamekuwa yakisogezwa mbele kila mwaka, kutokana na mipango kutokamilika kwa wakati.

Kampuni ya Total E&P Uganda ambayo ndiyo ilikua ikiongoza katika ujenzi wa bomba hilo imewatawanya wafanyakazi waliokuwa wakitarajiwa kuanza kazi hiyo.

Kampuni ya Cnooc Uganda Ltd ambayo inashiriki katika utafutaji wa mafuta nchini humo imewasimamisha kazi takrbani wafanyakazi 12, kufuatia kuchelewa kuanza kwa mradi wa bomba la mafuta.

Hata hivyo Kampuni ya Total haikuwa tayari kuzungumzia uamuzi huo.