Kampuni za mawasiliano ya simu zinavyoleta mapinduzi katika sekta ya afya

0
63

Wiki iliyopita Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford imetangaza mradi mkubwa wa afya nchini Tanzania. Mradi huo utakaogharimu shilingi za Kitanzania bilioni 13.5 unalenga kutumia teknolojia ya akili bandia za mifumo ya kompyuta kwa kimombo Artificial Intelligence (AI)na ugunduzi wa chanzo na athari za magonjwa kidijitali (digital pathology). Uwekezaji wa namna hii unasaidia kuhakikisha kwamba hospitali nchini Tanzania zinaendelea kujenga uwezo wa kutoa huduma bora zaidi.

Matumizi ya intaneti kupitia simu za mkononi na teknolojia ya mawasiliano kwa ujumla imeleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za afya. Mfano mmojawapo ni matumizi ya programu za simu kama zile za m-health. Programu hizi husaidia wagonjwa kufanya tafiti za awali za kinachowasumbua mtandaoni, kushirikisha dalili wataalamu na kupata orodha au njia za tiba. 

Mapinduzi haya ya teknolojia katika utoaji wa huduma ya afya yamesaidia pia utoaji huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na wagonjwa wa Kifua Kikuu. Huduma mbili za simu ambazo zimetambulishwa mwaka jana kwa watu waishio katika mazingira hatarishi kiafya, hutoa msaada wa kutuma ujumbe mfupi (SMS) zenye mafunzo namna ya kuishi na magonjwa yao au kuzingatia tiba na nyingine hutuma hata SMS kukumbusha kuhusu muda wa kwenda hospitali au kumeza dawa. M-Health pia inasaidia watoa huduma za afya kusajili wagonjwa, kuhifadhi taarifa za afya na tiba na kuwasiliana. Mfano mwingine mkubwa wa huduma za afya kwa njia ya simu ni ule wa kampuni ya Tigo Tanzania wa kusajili watoto wanaozaliwa. Mfumo huu umeisaidia serikali kwa kiasi kikubwa na mpaka sasa umetumika kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa zaidi ya milioni 4.2.

Ili Watanzania waendelee kufaidi huduma hizi za kibunifu katika sekta ya afya, lazima sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi iendelee kukua kimtaji, kimiundombinu, kitaaluma na kifaida. Hili linawezakana kama tutaweka kipaumbele katika kuwa na sera bora zaidi siku hadi siku. 

Send this to a friend