Kampuni za simu zatozwa faini bilioni 2 kwa kukiuka kanuni za usajili wa laini

0
57

Kampuni zinazotoa huduma za simu zimetozwa faini ya shilingi bilioni 2.08 kwa kushindwa kutii kifungu kinachowataka kutotumia kitambulisho cha taifa kimoja kusajili zaidi ya laini tano kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 37 cha kanuni za usajili wa laini za simu cha mwaka 2023.

Hatua hiyo ni kufuatia mwezi mmoja tangu ripoti ya robo ya nne ya mwaka 2023 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kubaini matukio ya ulaghai 21,788 yakiongezeka kwa asilimia 73 kulinganisha na matukio 12,603 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, kampuni zilizotozwa faini ni Airtel Tanzania Plc, Honora Tanzania Limited (Tigo), Viettel Tanzania Plc (Halotel), Vodacom Tanzania Plc na Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ambazo zilibainika kukiuka kanuni hizo kuanzia mwezi Septemba hadi Novemba 2023.

Aidha, ripoti zinaeleza kuwa kampuni ya Airtel iliruhusu jumla ya laini 26,009 kusajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya taifa 6,165 pekee, hivyo kutozwa faini ya shilingi bilioni 1.541, Tigo imetozwa shilingi milioni 473 kwa kutumia vitambulisho 1,892 kusajili laini nyingi kuliko kuliko inavyotakiwa.

Vilevile Halotel italazimika kulipa faini ya shilingi milioni 50.5 kwa kutumia vitambulisho 202 kusajili laini nyingi zaidi ya inavyotakiwa, Vodacom italazimika kulipa faini ya shilingi milioni 14.75 baada ya vitambulisho 59 kutumika kusajili laini nyingi, huku TTCL ikilazimika kulipa shilingi milioni 5 baada ya vitambulisho 12 kutumika kusajili kinyume na kanuni.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend