Kanisa Katoliki la Kiaskofu Geita lafungwa kwa kupoteza hadhi  

0
18

Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita limefungwa kwa muda kufuatia uvamizi na uharibufu wa mali katika eneo la Altare usiku wa kuamkia Februari 26, 2023.

Askofu wa Jimbo  Katoliki, Flavian Kassala amethibitisha kufungwa kwa kanisa hilo kuanzia Februari 27, mwaka huu kutokana na uharibufu  wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ulioivunjia heshima yake pamoja na unajisi kwa utakatifu wa jengo hilo la kanisa.

“Kutokana na matukio hayo, Kanisa hili limepoteza kwa kiasi kikubwa baraka yake na jamii ya waamini imeumizwa sana kutokana na kashfa, kufuru na unajisi uliofanyika kwa imani yetu.

Hivyo naagiza kwamba Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo Katoliki la Geita halistahili kwa maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi, wala ya Sakramenti yoyote, wala kwa ibada yoyote,” amesema

Aidha, amesema kufuatia hali hiyo kanisa limefungwa kwa huduma zote za kiibada kuanzia Februari 27 hadi Machi 18, 2023 ili kusubiri utakaso wake.