Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma limekifikisha mahakamani Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali katika shauri la mgogoro wa ardhi kwa madai ya kuporwa eneo lao.
Bodi ya wadhamini wa kanisa hilo imefungua shauri hilo Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CCM, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Shauri hilo lililofunguliwa kwa dharura limedai kuwa Waziri wa Ardhi na Halmashauri ya Uvinza tayari wamepanga kukipatia chama hicho ardhi hiyo kwa ajili ya kujenga madarasa bila ridhaa ya mwenye eneo hilo.
Kanisa hilo limeiomba mahakama itoe amri ya zuio la muda ya upande mmoja dhidi ya wadaiwa na mawakala wao kutokujihusisha na jambo lolote katika eneo hilo kusubiri usikilizaji na kuamriwa kwa maombi hayo pande zote.
Rais Samia ataka sheria zinazochelewesha haki zifanyiwe marekebisho
Aidha, kanisa limewapatia wadaiwa taarifa ya siku 90 ya nia ya kuwashtaki, kwa mujibu ya Sheria ya Mashauri dhidi ya Serikali, muda ulioanza Desemba 7, 2022 hivyo kuiomba mahakama kutoa amri yoyote inayofaa.
Akizunguma na Mwananchi wakili wa kanisa hilo, Method Kabuguzi amesema shauri hilo limepangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lameck Mlacha na hivyo itatajwa Februari 15, 2023.