Kanuni 5 zitakazotumika kwenye Kikokotoo kipya kuanzia Julai 2022

0
42

Serikali imeridhia maombi ya wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii kwa kupandisha asilimia ya kikokotoo kutoka 25% iliyolalalamikiwa mwaka 2018 mpaka 33% kuanzia Julai Mosi 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu ametangaza rasmi kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni kufuatia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoelekeza mnamo kuhusu mapendekezo ya kanuni ya Mafao ya wastaafu iliyoombwa na TUCTA Mei mosi, 2022.

Alisema kuwa Kanuni hiyo mpya ambayo imetangazwa ina manufaa mengi ikiwemo Mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF itaimarika na kuwa endelevu, kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi asilimia 33, kuongeza pensheni ya mwezi kutoka asilimia 50 ya sasa hadi asilimia 67 kwa waliokuwa wanachama wa PSPF na LAPF ambao ni asilimia 19 ya wanachama wote wa mifuko ya pensheni.

Manufaa mengine ni kuwa mifuko itaweza kuongeza pensheni ya kila mwezi kwa kuzingatia tathmini zitakazofanyika kila baada ya miaka mitatu, pamoja na wanachama wote wanaochangia kwenye mifuko ya pensheni watatumia kanuni moja ya mafao na hivyo kuweka uwiano na usawa wa mafao baina ya Wastaafu.

Amefafanua kuwa, kanuni hiyo mpya itakuwa na vikokotoo vifuatavyo; Kiwango cha mkupuo kitakuwa cha asilimia 33 kwa mifuko yote, kikokotoo limbikizi kitakuwa 1/580 kama ilivyo kwa Mfuko wa NSSF na iliyokuwa mifuko ya PPF, GEPF na baadhi ya wanachama wa iliyokuwa PSPF na LAPF, makadirio ya miaka 12.5 ya kuishi baada ya kustaafu kama ilivyo kwa Mfuko wa NSSF na iliyokuwa Mifuko ya PPF, GEPF na baadhi ya wananchama wa iliyokuwa PSPF na LAPF, mshahara wa kukokotoa mafao ya pensheni utakuwa wastani wa mishahara bora ya miaka mitatu ndani ya miaka 10 kabla ya kustaafu na umri wa kustaafu kwa lazima utaendelea kuwa miaka 60.

Ameongeza kuwa, pensheni za wastaafu watakaotumia kanuni hizo zitakuwa zikihuishwa mara kwa mara kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uwezo wa mifuko ya pensheni.

Wakati huo huo, rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema kuwa zoezi la uandaaji wa Kanuni mpya ya Mafao ya pensheni ilikuwa shirikishi ambapo vyama vya wafanyakazi, waajiri nchini na Serikali kwa pamoja wameweza kufanikisha hayo kwa ajili ya kuhakikisha uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii na wanachama kupata mafao yao.

Send this to a friend