Karani atakayepoteza kishkwambi kukatwa kwenye malipo yake
- Serikali kukata gharama za vishkwambi kwa makarani waliopoteza vishkwambi kwenye malipo yao ya mwisho.
- Karani aliyepoteza kishkwambi hataathiri zoezi la Sensa kwakuwa vipo vya akiba.
Kutokana na kuwepo kwa upotevu wa baadhi ya vishkwambi vinavyotumiwa na makarani wa Sensa kwaajili ya kukusanyia taarifa, Serikali imesema watakaopoteza vifaa hivyo watakatwa kwenye sehemu ya malipo yao.
Ameyasema hayo Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Spika Mstaafu Anne Makinda wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Makarani wawili wa Sensa waporwa vishkwambi vya Sensa
“Waliopoteza vishkwambi hawataathiri Sensa kwa kuwa vipo vya akiba, lakini wajue watakatwa malipo yao ya mwisho kufidia vilivyopotea,” amesema Makinda.
Aidha, amefafanua pia kuhusu karani wa Sensa aliyedaiwa kujifungua Agosti 22, mwaka huu siku moja kabla ya kuanza zoezi hilo wilayani Bunda, Mkoa wa Mara na kuthibitisha kuwa taarifa hizo ni za kweli.
“Ni kweli yupo karani amejifungua usiku wa kuamkia siku ya Sensa, hivyo kutuongezea mtu mmoja na watu wa haki za binadamu, nimeona wanahoji na kuleta ukakasi, wapo walioomba hii kazi online (mtandaoni) na kuthibitishwa na kata zao, kama yalitokea mapungufu tumerekebisha,” ameeleza.