Jeshi la Polisi limewakamata watu wawili, Frank Mbetu (35) mkazi wa Ligula, Mtwara na Honest Mgona (47) mkazi wa Mabwepande kwa kujifanya watumishi wa serikali na kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema mtuhumiwa Frank Mbetu alijifanya mtumishi wa Serikali ngazi ya Katibu Mkuu Kiongozi na kuwalaghai watu kuwa angewapa kazi serikalini au kupandishwa vyeo, huku Mgona akijifanya kuwa ametumwa na Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kusambaza mitungi ya gesi kwa wananchi na baadaye kuwatapeli kwa kuwadai pesa za usafiri.
Aidha, Polisi wanamshikilia Edwin Kasebele (24) mkazi wa Mapelele, Mbeya kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa ‘Facebook’ na ‘Whatsapp’ kuwa anafanya biashara ya vitenge na hivyo kujipatia pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali.
Watano wakamatwa kwa uchochezi mtandaoni dhidi ya viongozi wa Serikali
“Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na simu saba na kadi za simu 13 za kampuni mbalimbali za simu ambazo wamekuwa wakitumia kama nyenzo kutekeleza uhalifu wao,” amesema Kamanda.
Mbali na hayo, Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao na kuwahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwenye kituo cha Polisi kilicho karibu ili hatua stahiki zichukuliwe haraka.