Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Juni 11, 2021 ametangaza kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila siku chache baada ya kumteua kwenye wadhifa huo.
Kutenguliwa kwa Chalamila kumekuja siku mbili kabla Rais Samia hajaanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani humo ambapo atakagua miradi ya maendeleo.
Pengine anguko la Chalamila si jambo ambalo litawashitua wengine kwani tayari kulikuwa na dalili hiyo kutokana na aliyoyasema Rais siku ya kuwaapisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala ambapo alisema kiongozi huyo ni mlipukaji.
“Nimewasimamisha ma-RC na ma-RAS ili tuone shughuli itakavyokuwa huko mfano pale Mwanza nimesema ni kiberiti na petroli kwa sababu ni Samike (RAS) mkimya lakini ana zake, yule mwingine RC Chalamila ni mlipukaji,” alisema Rais.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila ni kiberiti, yeye ni mlipukaji- Rais Samia Suluhu Hassan pic.twitter.com/AAJzuGzKWp
— Swahili Times (@swahilitimes) June 2, 2021
Licha ya kuwa taarifa ya utenguzi wa Chalamila haijaeleza sababu ya uamuzi huo, lakini unahusishwa na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye ziara za Rais na waje na mabango hata yenye matusi.
“… tuweze kumpokea Mheshimiwa Rais wetu kwa mabango mengi, mabango ya aina yoyote, hata kama ataandika tusi, aandike. Yoyote yale,” alisema Chalamila akitoa wito kwa wananchi.
Aprili 6, 2021 akiwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, Rais Samia alisema kuwa viongozi wahakikishe wanatatua changamoto za wananchi katika ngazi zao na kwamba mabango yanayobebwa kwenye ziara za viongozi wakuu yawe tu ni yale mambo ya kitaifa.
Alisema akikuta bango moja linalohusu changamoto isiyo ya kitaifa, mkuu wa wilaya au mkurugenzi ataondoka, kwani ni ishara kuwa ameshindwa kutimiza wajibu wake.
Kufuatia utenguzi huo, Rais amemhamisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhandisi. Robert Luhumbi kwenda kuwa Mkuu Mkoa wa Mwanza.
Katika ziara yake mkoani Mwanza, Rais Samia atakagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi ambalo ujenzi wake unagharimu TZS bilioni 700 na kuzindua mradi wa maji wilayani Misungwi.
Pia, atazindua jengo la Benki Kuu ya Tanzania na kukutana na vijana kwa niaba ya vijana wote wa Tanzania.