Kauli ya Rais Dk Magufuli kuhusu uzuiaji wa mifuko ya plastiki

0
45

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Watanzania kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuacha kutumia mifuko ya plastiki ambayo ina madhara makubwa katika mazingira na viumbe hai wakiwemo binadamu.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 03 Juni, 2019 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la samaki la Feri Jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kushtukiza sokoni hapo na kujionea wafanyabiashara na wanunuzi wa samaki wakitumia mifuko mbadala.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wote ambao wamesimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa tangu mwaka 2016 kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kutotumia mwanya huo kuuza mifuko na vifungashio  mbadala kwa bei kubwa na badala yake amewataka wafanyabiashara hao pamoja na wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vya kutengeneza mifuko na vifungashio kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuwa na vifaa vya kubebea bidhaa wanazozinunua madukani na masokoni ili kuepuka gharama kununua vifungashio ama mifuko mbadala.

Mhe. Rais Magufuli ameziagiza mamlaka zinazohusika, kuhamasisha utengenezaji wa mifuko na vifungashio mbadala hapahapa nchini ili kuongeza ajira katika viwanda vya kutengenezea bidhaa hizo badala ya kuacha wafanyabiashara wakigeuza nchi kuwa mahali pakuingiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Akiwa katika soko hilo la Feri, Mhe. Rais Magufuli amenunua samaki kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia vitambulisho vya wajasiriamali na amewapongeza kwa juhudi zao za kujitafutia kipato halali.

Ameiagiza Manispaa ya Ilala kupunguza tozo ya pango kwa wapaa samaki kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 500 kwa siku na ameitaka manispaa hiyo kutenga shilingi Milioni 10 kutoka kwenye makusanyo ya soko hilo kujenga jengo jingine la wafanyabiashara wasiouza samaki kama vile Mama Lishe, Baba Lishe na wauza bidhaa zingine ambao hawanufaiki na jengo la wauza samaki ambalo mwaka jana alichangia shilingi Milioni 20.

Mhe. Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wauza samaki ambalo alilichangia shilingi Milioni 20 mwaka jana ambapo ameagiza Manispaa ya Ilala ifanye ukaguzi wa gharama zilizotumika kutokana na kuwepo wasiwasi wa matumizi mabaya ya fedha.

Ameiagiza Manispaa ya Ilala na Menejimenti ya soko la Feri kuweka utaratibu wa kuwapokea wafanyabiashara wanaoingiza samaki sokoni hapo kwa muda wote wa saa 24, kuweka umeme na maji katika jengo mojawapo la wafanyabiashara wa samaki ndani ya siku 5 na kuingiza umeme katika jengo la huduma ya Msalaba Mwekundu (Red Cross) lililopo sokoni hapo.

Huku wakimshangilia Wafanyabiashara wa soko la Feri wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jinsi anavyowapigania Watanzania wanyonge wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wamemhakikishia kuwa watatekeleza maagizo yake ya kutotumia mifuko ya plastiki kama inavyoelekezwa katika sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

03 Juni, 2019

Send this to a friend