Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza kuwa nchi yake itaondoa mahitaji ya visa kwa wageni wote duniani kuanzia Januari 2024 ili kufungua mipaka kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akizungumza katika sherehe za uhuru wa miaka 60 jijini Nairobi, Ruto amesema kuanzia mwakani hakuna atakayelazimika kutuma maombi ya kupata visa kwa ajili ya kutembelea nchi hiyo.
Aidha, ili kutekeleza sera hiyo, amesema mfumo wa kidijitali umeundwa kuhakikisha wasafiri wote wanaoelekea nchini Kenya wanatambuliwa mapema kupitia jukwaa la kielektroniki, na baada ya kutambuliwa, “wageni wote watapata idhini ya kusafiri ya kielektroniki.”
Ruto ambaye amekuwa akiunga mkono wazo la Afrika isiyo na mipaka, sasa anafanya Kenya kuwa nchi ya pili barani Afrika kufungua mipaka yake, baada ya Rwanda kufanya hivyo mwezi Novemba mwaka 2023.
Kabla ya hatua hii, Kenya ilikuwa tayari imewaondolea raia wa Indonesia mahitaji ya visa, na pia ilitangaza kuwa Comoros itasaini makubaliano kama hayo mwishoni mwa mwaka.