Kenya kuzalisha nishati ya nyuklia ifikapo 2038

0
16

Kenya inategemea kuwa na kinu cha kwanza cha kuzalisha nishati ya nyuklia ifikapo mwaka 2038 ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini humo.

Kulingana na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria na Udhibiti, na Katibu wa Shirika la Wakala wa Nishati ya Nyuklia (NuPEA), Justus Wabuyabo kinu cha nyuklia cha megawati 1,000 kitaanza kutumika ifikapo mwaka 2038.

Nchi hiyo inatazamia kujenga vinu zaidi ili kupunguza uhitaji wa umeme katika siku zijazo ambapo NuPEA imetia saini mkataba na China, Urusi, Korea Kusini na Slovakia kwa ajili ya mafunzo ya nyuklia kwa wafanyakazi wake.

“Kama nchi, tumekubali faida zinazowezekana za kutumia nishati ya nyuklia na tumechukua uamuzi wa kisera kuijumuisha kama chaguo la teknolojia katika sera yetu ya kitaifa ya nishati,” amesema Wabuyabo.

Wabuyabo anasema tangu 2010, Kenya imeonesha nia ya kuendeleza programu za nishati ya nyuklia ili kuongeza upungufu uliopo wa umeme, na kwamba nishati hiyo ni salama, rafiki kwa mazingira na yenye ushindani kiuchumi ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati.

Amewatoa hofu Wakenya kuwa hawapaswi kuogopa kuhusu nishati hiyo kwa kuwa hatua za kiufundi za kupunguza hatari ya ajali au viwango vya mionzi kwa mazingira zimekwisha angaliwa.