Taharuki ilizuka ndani ya Bunge la Kenya jana baada ya mbunge mmoja kuingia na bastola ndani ya ukumbi wa bunge wakati kikao kikiendelea.
Mbunge Elisha Odhiambo alimtaarifu spika kuwa ameona kitu kama bastola ndani ya koti la mbunge mwenzake, Mohamed Ali.
Spika Justin Muturi alimtaka Ali kuthibitisha kama kweli ameingia na silaha ndani ya ukumbi.
“Samahani, nilisahau kuiacha nje, mimi pia ni binadamu. Spika naomba uniruhusu niiikabidhi,” alisema mbunge huyo.
Spika amewataka walinzi wa ukumbi huo kutimiza wajibu wao, akisema kitendo cha kiongozi huyo kupita na silaha ni ishahara kuwa wamekuwa wazembe.
Hata hivyo Ali alimkosoa mbunge mwenzake kwa kutangaza kuwa alikuwa na silaha na kusema hiyo ni chuki ya kisiasa kwani wanatokea vyama tofauti.
Mbunge mwingine, Millie Odhiambo amesema nchi hiyo ipo katika mgogoro wa kisiasa na hivyo ametaka kanuni za ulinzi zifuatwe.
Wabunge nchini humo wamegawanyika kufuatia mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ambapo pia Rais na Makamu wa Rais wako pande tofauti za mabadiliko hayo.