Askari Polisi aliyekuwa akilinda kituo cha kuwaweka watu wenye maambukizi ya virusi vya corona (karantini) katika Kaunti ya Busia nchini Kenya amekamatwa baada ya kukutwa akijamiiana na mmoja wa waathirika.
Kituo cha Mafunzo ya Kilimo (ATC) walipo waathirika hao hulindwa na polisi wakati wote kwa sababu kinatumiwa na wananchi wa kawaida pamoja na wafungwa kutoka Gereza la Busia wenye maambukizi ya COVID19, lakini makundi hayo huwekwa kwenye wodi tofauti.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Busia amesema kuwa Alhamisi majira ya saa nne usiku mmoja wa askari hao, Emmanuel Ng’etich alionekana akizungumza na muathirika mmoja, na ndipo mlinzi mwenzake akaamua kwenda kuwaeleza wenzake kinachoendelea, lakini waliporudi hawakumuona Ng’etich.
Taarifa iliyowasilishwa polisi imeeleza kuwa askari hao alianza kumtafuta na baada ya muda walisikia sauti kutoka kwenye wodi ya wanawake, na polisi walipofika hapo waliwakuta wanawake hao wakiwa nje wakidai kuwa Ng’etich alikuwa akimbaka mwenzao.
Mamlaka zimesema kuwa walipoingia ndani waliwakuta wawili hao wakiwa utupu kitandani.
Mmoja wa wanawake waliopo karantini ameliambia jeshi la polisi kuwa si kweli kwamba Ng’etich alimbaka mgonjwa huyo, kwani walikubaliana kujamiina na mwanamke huyo amebadili maelezo baada ya wenzake kujua kitendo alichokifanya.
Kufuatia tukio hilo Ng’etich amekamatwa na kuwekwa karantini katika kituo hicho hicho na sampuli imechukuliwa kwa ajili ya kupimwa kama ana maambukizi.