KENYA: Serikali yafukua kaburi na kumvua marehemu sare ya kazi aliyozikwa nayo

0
35

Maafisa wa serikali ya Kaunti ya Kakamega iliyopo Magharibi mwa Kenya wamefukua mwili wa mwanaume mmoja ili kutoa sare za kazi alizozikwa akiwa amezivaa.

Martin Shikuku Alukoye alizikwa akiwa amevaa sare za kazi (Kakamega County Youth Service uniform) baada ya kufariki dunia kufuatia kuzama mtoni Agosti 7 mwaka huu.

Mwili wa mwanaume huyo mwenye miaka 31 umefukuliwa baada ya kuwa alizikwa Agosti 11 akiwa na sare hizo za kazi.

Ndugu wa marehemu wamesema kuwa kitendo cha kufukua kaburi la ndugu yao kimefanywa kinyume na sheria, na tamaduni za kwao, kwani wafukuaji walitakiwa kuwa na kibali cha mahakama kabla ya kufanya hivyo.

Familia ya marehemu imesema kuwa iliishirikisha serikali ya kaunti katika mchakato mzima wa maziko ya ndugu yao, ikiwa ni pamoja na ombi la kumzika akiwa na sare hizo yambo ambalo lilikubaliwa.

Wazee wa eneo hilo wamekosoa kitendo hicho ambacho wamesema ni kuukosea heshima mwili wa marehemu, na pia ni jambo ambalo linakiuka mila za ukoo wa Abang’onya.

“Tualazimika kumzika mtoto wetu wakati wa usiku kwa sababu kwa mujibu wa mila zetu, mtu aliyefariki kwa kuzama kwenye maji hatakiwi kuzikwa kukiwa na jua, sasa tunashangaa maafisa wa serikali kuja kufukua mwili wa mtoto wetu ili kuchukua nguo,” alisema mmoja wa wazee wa eneo hilo.

Mwili huo ulivikwa nguo nyingine na kisha kuzikwa tena baada ya wazee wa kimila kufanya kile walichodai ni kuisafisha familia hiyo.

Send this to a friend