Kenya: Ugumu wa uchumi wasababisha mamilioni kukata tamaa ya kutafuta kazi

0
39

Takwimu kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu nchini Kenya (KNBS) zimebainisha kuwa theluthi mbili ya watu wasio na kazi wamekata tamaa kutafuta kazi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi unaopelekea kampuni kusitisha kuajiri ili kujikimu.

Kulingana na takwimu za KNBS, kati ya jumla ya Wakenya milioni 2.97 wasio na kazi wenye umri wa kati ya miaka 15 na 64 ambao ni nguvu kazi, milioni 2.01 hawakuwa wakitafuta kazi kikamilifu, huku idadi ya wahitimu au walioachishwa kazi ambao wamekata tamaa kutafuta kazi ikiongezeka, na hivyo kuchangia asilimia 67.71 ya watu wasio na ajira.

Wengi wa wale ambao wamekata tamaa ya kuajiriwa ni wenye umri wa kati ya miaka 20 na 24, wakifuatiwa na wenye umri wa miaka 25 hadi 29. Idadi ya watu wenye umri wa miaka 20-24 ina wahitimu wengi wapya ambao juhudi zao za kutafuta kazi zinadhoofishwa na kukosekana uzoefu.

Kenya: Wananchi waacha magari majumbani kutokana na bei kubwa ya mafuta

Idadi kubwa ya washiriki wapya katika soko la ajira kila mwaka pia imesababisha fursa finyu, na kuwalazimu wengi kutafuta njia mbadala kama vile kuanzisha biashara ndogo ndogo.

Tangu Machi 2020, kampuni nyingi zimekuwa zikisita kuchukua wafanyakazi zaidi kutokana na kudorora kwa uchumi uliochangiwa na janga la UVIKO-19, ambalo lilisababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi na mishahara.

Wachumi nchini humo wamedai katika miaka ya ukuaji wa uchumi wa Kenya imeunda nafasi za kazi lakini nyingi ni za malipo ya chini na zisizo rasmi, huku Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri wa Kenya, Jacqueline Mugo akinukuliwa kuwa “kwa wastani, nchini Kenya, watu wanakaa bila ajira kwa miaka saba.”

Chanzo: Business Insider Africa

Send this to a friend