Viongozi sita wa Azimio la Umoja, akiwemo Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo, huenda wakahukumiwa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kufikishwa mahakamani Alhamisi Machi 23, 2023 kwa kosa la kushiriki maandamano siku ya Jumatatu, Machi 20.
Viongozi hao walishtakiwa kwa kushiriki katika mkusanyiko usio halali pamoja na kuharibu gari la Volkswagen Passat.
Wajumbe wawili wa Mabunge ya Kaunti waliachiliwa Jumatatu jioni baada ya kukamatwa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali jijini Nairobi, na kuamriwa kufika mahakamani Alhamisi Machi 23, kwa ajili ya kusomewa mashtaka rasmi.
Odinga: Tutafanya maandamano kila Jumatatu
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliiambia mahakama kuwa Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi walikuwa miongoni mwa viongozi sita waliokiuka Sheria ya Utaratibu wa Umma.
Wandayi na Madzayo walikamatwa katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) walipokuwa wakijaribu kuandaa maandamano dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.
Mnamo Jumapili Machi 19, Kamanda wa Mkoa wa Nairobi, Adamson Bungei alimuonya kiongozi wa Muungano wa Umoja One wa Kenya, Raila Odinga kwamba maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumatatu na Alhamisi ni kinyume cha sheria za nchi.