Kenya: Wanafunzi 4,000 wapata mimba miezi 4 iliyopita

0
19

Idara ya Watoto katika Kaunti ya Machakos nchini Kenya imeeleza kuwa takribani wanafunzi 4,000 wenye umri chini ya miaka 19 wamepata ujauzito ndani ya miezi minne iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari, afisa kutoka idara hiyo, Salome Muthama amesema vitendo hivyo vimeongezeka kutokana na janga la corona lililopelekea shule kufungwa.

Taarifa ya Muthama inaonesha kuwa watoto waliopata ujauzito ni kati ya wenye umri wa miaka 10 hadi 19.

Muthana amewatuhumu wazazi kwa kuwatelekeza watoto, ambapo amewataka kuchukua hatua kwa sababu wengi waliohusika kuwapa watoto ujauzito ni ndugu wa karibu.

Afisa huyo ameisihi mahakama kuipatia idara hiyo washauri wa kisheria ili kuwezesha kuharakisha michakato ya kesi zinazowahusu watoto.

Aidha, Serikali ya Kaunti ya Machakos imekanusha takwimu hizo kwa madai kuwa hazijathibitishwa, huku wakitaka uchunguzi zaidi ufanyike.

“Ni vigumu kuwa na idadi kubwa kiasi hicho ndani ya miezi michache,” amesema afisa anayehusika na elimu na kuongeza kuwa hospitali ndipo sehemu sahihi ya kupata takwimu.