Kenya: Wananchi waiba mafuta ya transifoma na kutumia kupikia

0
46

Mamlaka ya nishati nchini Kenya imesema kuwa inapoteza mamilioni ya dola kwa mwezi kutokana na uharibifu wa transfoma zake za umeme ambazo mafuta yake huibwa na kuuzwa kama mafuta ya kupikia.

Taarifa ya mamlaka hiyo inaeleza kuwa wahalifu huchota mafuta hayo kutoka kwenye transfoma, kisha huuzwa na makampuni makubwa kwenye migahawa na vibanda vilivyo kando ya barabara kwa ajili ya kupikia chakula.

Ongezeko la hivi karibuni la uharibifu wa mali hizo limehusishwa na kupanda kwa gharama za mafuta ya kupikia, huku Wataalamu wa afya wakionya kuwa mafuta ya transfoma ambayo yanaonekana kama mafuta ya kupikia,  si salama kwa matumizi ya binadamu na yana hatari kubwa kiafya.

Aidha, kumekuwepo matukio ya watu kujeruhiwa kwa shoti ya umeme wakati wakijaribu kuiba mafuta hayo.

Kampuni hiyo  sasa imeanza kampeni ya uhamasishaji nchi nzima kuhusu hatari ya kuharibu gridi ya taifa  ambapo karibu transfoma 20 zimeharibiwa, huku takribani watu 22 wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka.