Kenya yabaini uwepo wa aina (strains) tisa za virusi vya corona

0
38

Taasisi ya Utafiti wa Tiba nchini Kenya (KEMRI) imethibitisha uwepo wa angalau aina (strains) tisa za virusi vya corona vinavyosambaa nchini humo.

Ripoti ya uchunguzi huo iliyolenga kufuatilia mabadiliko (mutations) ya virusi vya corona inaeleza kuwa aina hizo zilizothibitishwa hazina tofauti na ambazo zimekuwa zikisambaa maeneo mbalimbali duniani.

Timu ya wanasayansi ilichambua jenomu (genomes) 122 zilizokusanywa kutoka kwa wagonjwa wenye dalili na wasio na dalili jijini Nairobi na mjini Mombasa.

“Uchambuzi unaeleza zaidi kuwa maambukizi yaliyobainika na kuthibitika mwezi Machi 2020 kwa kiasi kikubwa yalitokana na virusi kutokana nje ya nchi,” ripoti ya KEMRI inaeleza.

Sampuli za uchunguzi zilikusanywa kutoka katika visa vilivyothibitishwa nchini humo kati ya Machi 12 hadi Mei 25 mwaka huu.

Mkuu wa taasisi hiyo, Prof. Yeri Kombe amesema kuwa uchunguzi huo utawezesha kufuatilia kwa karibu mabadiliko ya virusi, hivyo kuwezesha kubaini chanzo cha maambukizi ndani ya jamii.

Hadi Juni 3, 2020 nchi hiyo ilikuwa imeripoti jumla ya visa 2,216 kati ya watu 85,058 waliopomwa.

Send this to a friend