Kenya yachaguliwa kuwa mjumbe kwenye baraza la Umoja wa Mataifa
Kenya imetangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya mjumbe asiye wa kudumu katika Barazala la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) baada ya kupata kura 129 dhidi ya Djibouti iliyopata kura 62.
Katika mzunguko wa pili wa kura uliofanyika Juni 18, 2020 jumla ya nchi 191 zilipiga kura.
Mzunguko wa kwanza wa zoezi la kutafuta mjumbe wa baraza hilo kutoka Afrika ulifanyika Juni 17, 2020, lakini mshindi hakupatikana baada ya nchi zote mbili kushindwa kupata mbili ya tatu (kura 128) ya kura zote. Kenya ilipata kura 113 huku Djibouti ikijizolea kura 78.
Ushindi huo unaifanya Nairobi kurudi (kuanzia Januari 2021) katika chombo hicho chenye nguvu duniani baada ya miaka 23. Kenya sasa itakuwa miongoni mwa wajumbe watakaoshiriki kufanya maamuzi ya masuala mbalimbali yahusuyo amani na ulinzi duniani.
Miongoni mwa maamuzi yanayofanywa na baraza hilo yanahusu kuweka vikwazo, kuruhusu matumizi ya nguvu ili kulinda amani pamoja na kuchagua majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Kenya imepata nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Umoja wa Mataifa (AU) kutokana na ushiriki wake katika ulinzi wa amani, lakini Djibouti ilikataa pendekezo hilo na kuamua kushindana (na Kenya) katika sanduku la kura.
Katika taarifa yake kwa umma, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameishukuru AU kwa kuipa nafasi nchi hiyo, lakini pia ameishukuru Djibouti kwa kuwa mpinzani mwenye nguvu.
Aidha, amesema ushindi huo unadhihirisha kukua kwa ushawishi wa taifa lake katika jumuiya ya mataifa na mshiriki wa kutegemewa katika maendeleo.
Kwa upande wake Rais wa Djibouti, Ismail Omar Guelleh ameipongeza Nairobi kwa ushindi huo na kusema anaamini itakuwa na uwakilishi wenye tija.
Mbali na Kenya, nchi nyingine zilizochaguliwa ni India, Mexico, Ireland na Norway.