Kenya yafichua mashirika yanayofadhiliwa na Ford Foundation kuchochea vurugu

0
63

Serikali ya Kenya imeiandikia rasmi barua Shirika binafsi la Kimarekani, Ford Foundation ikiituhumu shirika hilo kufadhili maandamano ya Kenya pamoja na kuyaweka wazi mashirika 16 ya Kenya yanayofadhiliwa na shirika hilo.

Katika barua iliyoandikwa kwa Darren Walker, Rais wa Ford Foundation, serikali ya Kenya kupitia Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje, Korir Sing’Oei imeeleza kwamba baadhi ya wapokeaji wa misaada kutoka kwa shirika hilo huenda wanachochea maandamano yanayoendelea nchini humo.

Barua hiyo inaeleza kwamba, kati ya Aprili 2023 na Mei 2024, wapokeaji kadhaa wa misaada wasio wa kiserikali, wakiwemo Africa Uncensored Limited, Kenya Human Rights Commission na Transparency International, walipokea jumla ya dola za Marekani milioni 5.78 [TZS bilioni 15.5] kutoka kwa Ford Foundation.

Serikali imeeleza wasiwasi wake kwamba, misaada hiyo inaweza kuwa inatumika kwa njia ambayo inachochea vurugu na maandamano yanayoendelea, ambayo yamesababisha uharibifu wa mali na kupoteza maisha.

Zaidi ya hayo, serikali imesema kuwa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.49 [TZS bilioni 4] kilitolewa kwa haraka bila maelezo katika mwezi uliopita pekee jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa.

“Mtakubaliana kwamba fedha zilizotolewa kwa wapokeaji wasio wa kiserikali ni nyingi na lazima zitumike kwa busara kuhudumia malengo halali au hatari ya kutumiwa vibaya kusaidia shughuli mbaya,” barua hiyo imebainisha.

Aidha, barua hiyo imewatuhumu baadhi ya wapokeaji wa misaada kwa kushiriki katika shughuli zinazokiuka sheria za Kenya, ikiwemo uchochezi, lugha ya chuki, na uhamasishaji kwa kutumia taarifa za uongo, jambo ambalo linaweza kukiuka Sera ya Ford Foundation ya Kutojihusisha na Mambo ya Kisiasa.

Send this to a friend