Kenya yafuta posho za vikao za wabunge

1
0

Serikali ya Kenya inatarajia kuokoa takribani KSh milioni 381.2 (TZS bilioni 7.7) kutoka kwenye posho za vikao za wabunge na maseneta 416 kwenye Bunge la 13 baada ya kamisheni ya mishahara kuifuta.

Wabunge wa Kenya ambao ni 349 na maseneta 67 hulipwa posho sawa za vikao zenye thamani ya Ksh 5,000 (TZS 100,000) kila wanapokutana mara nne na mara tatu kwa wiki, mtawalia.

Hata hivyo wote 416 watapewa msaada wa fedha zenye thamani ya KSh milioni 10 (TZS milioni 200) ambazo zitatozwa kodi, kwa ajili ya kununua gari lenye uwezo wa injini isiyozidi 3000cc kila baada ya miaka mitano.

Lakini posho za vikao vya kamati za bunge hazijaondolewa ambapo kwa sasa mwenyekiti wa kamati analipwa TZS 300,000, makamu mwenyekiti TZS 200,000 na wajumbe TZS 160,000.

Katika hatua nyingine kamisheni hiyo imekataa ombi la wabunge kulipwa mshahara TZS milioni 23, sawa na majaji wa Mahakama ya Rufaa, na hivyo watabaki na kiwango cha sasa cha TZS milioni 14.

Spika wa Bunge, Justin Muturi ameituhumu kamisheni hiyo kutowatendea haki wabunge akisema kuwa vituo vya vya kazi ni viwili (bungeni na jimboni) lakini wao pekee ndio hawapewi posho ya nyumba, na kwamba uamuzi wa kufuta posho za vikao utaweka mazingira magumu Bunge kupitisha ajenda za Serikali.

“Kuna wabunge walioniambia kuwa wakichaguliwa katika bunge la 13 watakuja ukumbini kuandika majina na kisha wataondoka,” amesema spika.

Mbali na mkopo wa gari, wabunge hupewa posho ya safari, posho ya matengenezo ya gari ya TZS milioni 7, bima ya afya ya TZS milioni 200 wanapokuwa wamelazwa, TZS milioni 6 kwa wagonjwa wa nje, TZS milioni 1.5 ya uzazi na TZS milioni 1.5 ya matibabu ya meno.

More News

Send this to a friend