Kenya yakabiliwa na uhaba wa kondomu

0
48

Baraza la Taifa la Kudhibiti  UKIMWI nchini Kenya (NACC) limesema kuwa nchi hiyo inakabiliwa na uhaba wa kondomu ambapo mahitaji yake yanafikia milioni 480 kila mwaka huku akiba ya sasa ikiwa ni milioni 79 pekee.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kondomu Duniani katika Chuo Kikuu cha Kenya Coast Polytechnic mjini Mombasa, Mratibu wa NACC Kanda ya Pwani, Omar Mwanjama amesema nchi inakabiliwa na upungufu wa kondomu milioni 401, hatua ambayo imeathiri ugawaji wa bure wa bidhaa hiyo kwa watu wanaolengwa.

 “Hali imetulazimisha kuzingatia wale tu wenye uhitaji mkubwa, jambo ambalo limezua malalamiko. Nchi inajitahidi katika kushughulikia upatikanaji wake, ikilinganishwa na mahitaji,” amesema Mwanjama.

Hata hivyo, Gazeti la la Daily Nation liliripoti kuwa vituo kadhaa vya umma na hoteli nchini humo vinakabiliwa na uhaba wa kondomu kutokana na mvutano wa ushuru kati ya wafadhili na Serikali ya Kenya.

Serikali ya Kenya husambaza bure mipira takribani milioni 180 kila mwaka kupitia mpango ambao unafadhiliwa na Hazina ya Kimataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA).

 

Send this to a friend