Mamlaka ya anga ya Kenya imekubali Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kufanya safari zote za ndege za mizigo kwa mujibu wa ombi lililotolewa na Serikali ya Tanzania, kuanzia leo Januari 16, 2024.
Hatua hiyo imefuata baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kutangaza kusitisha kibali cha Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kufanya safari kati ya Dar es Salaam na Nairobi kutokana na nchi hiyo kukataa ombi la safari zote za ndege za mizigo lililotolewa na ATCL likitaka kufanya safari kati ya Nairobi na mataifa mengine, jambo lililotajwa kuwa kinyume na makubaliano ya mkataba wa ushirikiano wa huduma za anga kati ya Kenya na Tanzania.
Baada ya uamuzi huo uliotolewa na Serikali ya Kenya, TCAA imetangaza kurejesha kibali cha Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kufanya safari zake kati ya Jiji la Dar es Salaam na Nairobi.
“Kufuatia hatua hiyo, Mamlaka ya Anga ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafuta uamuzi wake wa tarehe 15 Januari 2024 na hivyo idhini ya shirika la ndege la Kenya Airways kufanya huduma kati ya Nairobi na Dar es Salaam, inarejeshwa mara moja,” imesema taarifa iliyotolewa na TCAA.