Serikali ya Kenya imewaruhusu Wafanyabiashara wa Tanzania kuingia nchini Kenya na kuwekeza bila sharti la kuwa na viza ya biashara, ikiwa ni hatua ya kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Uamuzi huo umetolewa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akihutubia jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Wafanyabiashara wa Kenya Jijini Nairobi na kuwahakikishia kuwa Serikali za nchi zote mbili zipo tayari kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji.
Aidha, ametoa wiki mbili kwa mawaziri wake kutatua vikwazo vilivyosababisha msururu wa magari katika mipaka ya Holili na Taveta na kumaliza mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa mahindi ya kutoka Tanzania kwenda nchini Kenya, na ametaka kuwepo kwa utaratibu utakaoruhusu vibali vinavyotolewa kwenye kila nchi kukubalika katika nchi nyingine.
Kwa upande wake Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasihi wafanyabiashara hao kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili wafanyabiashara wengi zaidi wa Tanzania wajitokeze kuwekeza nchini Kenya kama ambavyo wafanyabiashara wa Kenya walivyowekeza kwa kiasi kikubwa nchi Tanzania.
“Tanzania ipo tayari kupokea uwekezaji kutoka Kenya, milango yetu ipo wazi na mikono yetu ipo tayari kuwapokea, Serikali ipo tayari kuwa daraja la kuwezesha biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu. “
Kauli mbiu ya jukwaa hilo ni “kuboresha biashara, utalii na uwekezaji kati ya Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Afrika Mashariki kwa kutilia mkazo umoja wa forodha.”