Malori zaidi ya 600 yanayosafirisha bidhaa kutoka Tanzania yamekwama kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania (Namanga) kwa zaidi ya wiki moja na kusababisha hasara kwa madereva pamoja na mzozo mkubwa mpakani.
Malori hayo ambayo husafirisha mizigo ndani ya Afrika Mashariki, bado yapo safarini lakini kwa mujibu wa madereva hao, safari yao imekwama kutokana na kucheleweshwa kwa mchakato wa ukaguzi mpakani.
“Toka jumatatu gari iko ndani lakini bado hawajafanya utaratibu wa kuivusha na kwenye foleni nimemaliza siku tatu upande wa Kenya lakini hadi leo bado sijajua kama gari itavukishwa ama bado,” amesema Martine Mfinanga, dereva wa lori.
Wakala wa Vibali, Alex Sencha ameeleza kuwa changamoto hiyo inatokana na Kenya kutotekeleza makubaliano ya kufanikisha kituo kimoja cha ukaguzi.
“Kuna tatizo la utekelezaji kamili wa eneo moja la forodha kati ya Kenya na Tanzania, ambalo Watanzania wametekeleza, wameweka maofisa wao upande wa Kenya lakini kwa upande wetu wa Kenya hatujatekeleza, hawajaweka maofisa wetu upande wa Tanzania,” ameeleza.
Mamlaka kutoka Kenya na Tanzania pia zinahusisha hali iliyopo na ongezeko la idadi ya malori katika kituo hicho huku wakitoa wito kwa serikali za Kenya na Tanzania kupanua kituo hicho kwa nia ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka.