
Bodi ya Kudhibiti na Kusimamia Michezo ya Kubahatisha nchini Kenya (BCLB) imetoa agizo la kusitisha matangazo yote ya kamari na michezo ya kubahatisha kwenye vyombo vyote vya Habari kwa kipindi cha siku 30.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Jane Mwikali Makau, amesema uamuzi huo umetokana na wasiwasi kwamba baadhi ya watu wanaanza kuifanya kamari kama njia halali ya uwekezaji na njia ya haraka ya kupata utajiri.
Ameongeza kuwa matangazo ya kamari yanayorushwa kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa 4 usiku yanaathari kubwa hasa kwa watoto, ambao wanaanza kuzoea kamari na hatimaye kuwa wategemezi wa kamari.
Rema: Wazazi wa Nigeria hawawakemei watoto wanaochangia kipato kwenye familia
“Kwa kuzingatia haya, na kwa mujibu wa mamlaka ya kisheria chini ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha (Sura ya 131, Sheria za Kenya), Bodi ya BCLB inaagiza kusitishwa kwa matangazo yote ya kamari na ushuhuda wa watu maarufu katika majukwaa yote ya habari kwa muda wa siku thelathini kuanzia tarehe ya taarifa hii,” amesema.
Agizo hili linawahusu waendeshaji wote wa kamari waliopewa leseni, na linakataza aina zote za matangazo na shughuli za uhamasishaji, yakiwemo matangazo ya redio na runinga, mitandao ya kijamii, magazeti, mabango ya barabarani, magari yenye chapa, ujumbe wa simu (SMS), barua pepe na matangazo ya watu mashuhuri au watangazaji maarufu (influencers).