Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kuanza kusikilizwa Oktoba 6

0
127

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Oktoba 6, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru kukamilisha taratibu za awali za kisheria, ikiwemo mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi.

Mahakama Kuu pia imejiridhisha kuhusu namna Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilivyopokea na kuendesha shauri hilo katika hatua za awali kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mahakama imetupilia mbali mapingamizi mawili yaliyokuwa yamewekwa na Lissu dhidi ya Jamhuri, ikiwa ni pamoja na lile linalohusu uhalali wa hati ya mashtaka, na uhalali wa viambatanisho vya mashahidi vinavyoambatanishwa na hati ya mashtaka.

Mahakama imesema hakuna ushahidi unaoonesha kuwa hati ya mashitaka ilifanyiwa marekebisho kwani hati iliyosomwa mbele ya mshitakiwa ndiyo hiyo hiyo iliyowasilishwa Mahakama Kuu.

Akizungumza mahakamani, Wakili wa Serikali Deogratius Mahinyila amesema upande wa Jamhuri utawasilisha mashahidi 30 pamoja na vielelezo kadhaa ili kuthibitisha mashtaka dhidi ya Lissu.

Send this to a friend