Kiasi kikubwa cha dawa za kulevya katika historia ya Tanzania chakamatwa

0
51

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Tanzania (DCEA) imekamata kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphemine zikiwa kwenye vifungashio vya kahawa na majani ya chai, katika operesheni maalum iliyofanyika Dar es Salaam na Iringa kati ya Desemba 5 hadi 23, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo amesema tangu udhibiti uanze DCEA haijawahi kukamata kiasi kikubwa cha dawa kama ilivyo sasa na iwapo zingefanikiwa kuingia sokoni watu milioni 76.3 wangeathirika.

Kiasi hicho cha dawa kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya Methamphemine na kilogramu 1001.71 aina ya Heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni kwa jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa ambapo watu saba wamekamatwa, kati yao wawili ni raia kutoka bara la Asia.

Amesema dawa ya Methamphemine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na Cocaine.

Aidha, amesema kwa sasa mtaani hakuna dawa za kulevya, hivyo waraibu wa dawa hizo wamekimbilia kwenye matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya, jambo ambalo wameanza kuchukua hatua kulidhibiti.

Send this to a friend