Kidato cha sita kuanza mitihani Juni 29 mwaka huu

0
16

Siku moja baada ya Rais Dkt Magufuli kutangaza uamuzi wa serikali kufungua vyuo vyote na kuanza masomo kwa wanafunzi wa kidato cha sita, Waziri wa Elimu amesema kuwa mitihani itaanza Juni 29 hadi Julai 16 mwaka huu.

Waziri Prof. Joyce Ndalichako amesema hayo alipokuwa akitoa utaratibu kwa wanafunzi hao ambapo amesema kwa wale wanaosoma katika shule za bweni wanatakiwa kuanza kuripoti Mei 30 kwa ajili ya maandalizi.

Aidha, amesema kuwa mitihani ya kidato cha sita itakwenda sambamba na ile ya vyuo vya ualimu.

“Tumeliagiza Baraza la Mitihani Tanzania [NECTA] kuhakikisha mitihani ya kidato cha sita inapomalizika, matokeo yatoke kabla ya Agosti 31, 2020 ili tuendane na agizo la Rais Magufuli kwamba hawa wanafunzi waweze kujiunga na vyuo vikuu kama ambavyo ilikuwa imepangwa,” amesema Ndalichako.

Ameongeza kuwa tahadhari zote zitachukuliwa kwa ajili ya kuwalinda wanafunzi dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Taasisi za mafunzo nchini zilifungwa Machi 2020, ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya serikali ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19.