Kigamboni yaletewa ‘teksi za baharini’ kupunguza adha ya usafiri

0
1

Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Azam Marine zimetangaza ujio mpya wa vivuko utakaopunguza kwa kiasi kikubwa adha ya usafiri kwa wananchi wanaoelekea katika eneo la Kigamboni.

Akizungumza katika uzinduzi wa vivuko hivyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema vivuko vilivyozinduliwa Januari 22, 2025, vitaungana na vingine viwili ambavyo vinafanya kazi tayari na kufanya jumla ya vivuko kuwa vinne. Pia, amesema kufikia Mei mwaka huu, Azam Marine wataongeza vivuko vingine vinne na kufanya jumla ya vivuko kuwa vinane.

Ulega amesema kila kivuko kimoja kati ya vivuko hivyo vina uwezo wa kubeba abiria 250 kwa wakati mmoja na kutumia dakika sita kwa safari moja. Kwa wastani huo, ndani ya saa moja, kivuko kimoja kinaweza kubeba mpaka abiria 2500, hivyo kwa vivuko vinane, abiria zaidi ya 20,000 wanaweza kusafirishwa ndani ya saa moja.

“Historia imeandikwa. Huu ndiyo ushirikiano wenye manufaa baina ya serikali na sekta binafsi. Kipekee kabisa, naomba nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ubunifu wake na maelekezo yake kwetu kuhusu kushirikiana na sekta binafsi kuondoa kero za wananchi ndiyo zinaleta mambo kama haya,” amesema.

Ulega amesema historia ya taabu katika maeneo yanayohitaji vivuko nchini ni ya muda mrefu, akieleza namna Watanzania walivyokuwa wakitumia kamba kuvushana kwenye maeneo hayo lakini akasema nchi sasa imepiga hatua kiasi kwamba watu wanasafiri kwa starehe ikilinganishwa hapo nyuma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine, Abubakar Salim amesema ujio wa vivuko hivyo vipya unatarajiwa kupunguza muda wa kusubiri na kusafiri kwa abiria kutoka muda wa zaidi ya nusu saa na kuwa kati ya dakika tano mpaka sita.

Send this to a friend