Kijana achoma nyumba ya familia baada ya ugomvi na mama wa kambo

0
7

Familia moja katika kaunti ya Vihiga, eneo la South Maragoli nchini Kenya imeachwa bila makazi baada ya kijana wao wa miaka 22 kudaiwa kuchoma nyumba ya wazazi wake kutokana na mzozo wa mfuko wa kubebea vitu.

Kwa mujibu wa Rose Makungu, mama mlezi wa kijana huyo, ameeleza kuwa kijana huyo ambaye ni mtoto wa mume wake alimkasirikia kwa sababu aliruhusu mpwa wake kutumia mfuko wake wa kubebea mboga.

“Kwanza alinipa vitisho, kisha akaenda kuchoma nyumba ya familia yetu. Baadaye alirudi kwenye nyumba yake ya vyumba viwili, akaiwasha moto na kutoweka,” amesema Makungu.

Baba wa kijana huyo, Francis Odari, amesema amekuwa akimuonya kijana wake dhidi ya kumtusi mke wake na kusababisha vurugu nyumbani, akisema kijana huyo amesababisha mali zake kuungua huku majirani wakifanikiwa kuokoa mifugo.

Kwa sasa, familia hiyo haina makazi na Odari amesema hajui kijana wake alipo. Pia, ameomba viongozi wa eneo hilo na wahisani kuwasaidia, kwani hali ya baridi iliyopo kwa sasa inawafanya kuteseka zaidi.