
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Seven Kipara (38) mkazi wa Ipwizi kwa tuhuma za kupanga njama za kumuua mama yao mzazi, jaribio ambalo lilipelekea kumjeruhi kwa risasi mtoto wa miaka minne, Sinzo Jifwalo mkazi wa Kijiji cha Ipwizi.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema Seven Kipara na Jifaru Kipara wanadaiwa kumtuhumu mama yao aitwaye Kweji Lugembe (75) kuwa mshirikina anayewaua watoto na wadogo zao.
“Kutokana na imani hiyo, walipanga njama ya mauaji dhidi ya mama yao kwa kuwakodi wauaji kutoka Mkoa wa Lindi ambao ni Tabi Deus na Shija kwa makubaliano ya kuwalipa shilingi milioni tano,” imesema taarifa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa ilipofika Juni 8, mwaka huu, Tabi Deus (39) mkazi wa Kilwa Masoko mkoani Lindi na Shija walifika eneo la Mji Mdogo wa Mbalizi ambapo walipokelewa na mwenyeji wao Seven ambaye aliwapeleka kulala kwenye nyumba ya wageni iliyopo Mbalizi hadi Juni 10, 2025 ndipo mwenyeji wao aliwaonesha mazingira ya nyumbani kwa mama yao.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa katika jaribio hilo, mnamo Juni 13, mwaka huu saa 6:05 usiku katika Kijiji cha Ipwizi, Kata ya Mjele Wilaya ya Mbeya Mjini, mtoto Sinzo alijeruhiwa kwa risasi kwenye bega la kushoto na mdomoni na mtuhumiwa Tabi Deus.
Taarifa za awali zinaonesha kuwa mtoto huyo alikuwa amelala chumbani na bibi yake Kweji Lugembe, na ghafla walisikia mlipuko kutoka eneo la dirishani kisha mtoto huyo alikutwa amejeruhiwa.