Wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari Kisomachi, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia Mei 12, 2023 baada ya kuingia kwenye tenki la kuhifadhi maharage.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kileuwo wilayani humo, Godfrey Mrema amesema wanafunzi hao wanadaiwa kufariki kwa kukosa hewa wakati walipoingia kwenye tenki hilo kwa ajili ya kutoa maharage ya chakula shuleni hapo.
“Wanafunzi hao wote wana umri wa miaka 17, na uongozi wa shule umesema wote walifariki baada ya kuingia kwenye tenki kwa ajili ya kutoa maharage ya kupeleka stoo kwa ajili ya kupika,” amesema.
Mtoto wa miaka 14 ashtakiwa kwa madai ya kubaka mtoto mwenzake
Ameongeza kuwa taarifa kutoka shuleni hapo zinadai mwanafunzi wa kwanza alipanda kwenye pipa kwa kutumia ngazi, na kwa bahati mbaya alitumbukia na kuanza kupiga kelele, ndipo mwenzake akaingia kwa ajili ya kumuokoa lakini walikosa hewa, na hadi kutolewa walikuwa wamekwishafariki.
Aidha, Jeshi la Polisi mkoani humo limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ambapo hadi sasa linawashikilia watumishi watatu wa shule hiyo akiwemo mkuu wa shule, mwalimu wa zamu na mtunza stoo wa shule.