Kinana: Rais Samia hawezi kuuza bandari

0
39

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdurahman Kinana, amezungumzia mjadala wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam huku akiweka wazi kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoingoza haiwezi kuuza bandari hiyo na kuhoji Rais auze bandari kwa maslahi yapi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mkendo Musoma Mjini Kinana alianza kwa kueleza kuwa liko jambo la bandari linazungumzwa na mjadala mkubwa, unaendelea kuwa mrefu, mjadala mpana.

“Nataka niwahakikishie msiamini kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyekula kiapo eti atafanya jambo ambalo halina maslahi na nchi. Haiwezi kutokea, Rais ambaye tangu amechukua usukani amefanya mambo mengi mazuri, kwa nini aende kuuza bandari, sababu ni ipi?

Ili apate nini, ili iweje na ukisikiliza huu mjadala usikilizeni kwa makini na mmeshausikiliza, wote tunaoutetea, wanaopinga pamoja na wanaokosoa hakuna anayesema kwamba kusiwe na uwekezaji hata mmoja kwani wote wanakubali kwamba kuna haja ya kuwekeza na lengo ni moja tu kuongeza ufanisi na kuongeza mapato,” amesema.

Ameongeza wako wanaotetea mkataba na wametoa ushauri mzuri, serikali imesema itapokea kila ushauri utakaotolewa, Chama Cha Mapinduzi kimesema serikali isikilize, kwa hiyo serikali inasikiliza ushauri, inasikiliza hoja, haya yote yatafanyiwa kazi, haiwezekani Rais akapuuza haya yote.

Amefafanua kuwa uwekezaji huo ni wa kiuchumi hivyo unatakiwa kujadili kwa hoja, hoja itasikilizwa, hoja yako itajibiwa, pale itakapotakiwa kufanyiwa kazi itafanyiwa kazi kwa maslahi mapana ya nchi.

Send this to a friend