Kinana: Wapinzani jengeni hoja na si kumkejeli Rais

0
22

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana amewashauri na kuwakumbusha wanasiasa wa upinzani kuheshimu fursa ya maridhiano ya kisiasa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kinana amesema lugha za matusi, kejeli na dharau dhidi ya kiongozi wa nchi zinapaswa kuepukwa ili kutoa fursa ya kuendeleza maridhiano na kuijenga Tanzania kwa pamoja.

Ameyasema hayo mjini Tabora wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Mara, Simiyu na Tabora kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.

“Niwasihi ndugu hatukatai mtoe hoja, hatukatai mseme yale mnayotaka kusema lakini semeni kwa uungwana, zungumzeni kwa busara, jengeni hoja.

“Kusema Rais ana akili za matope au kusema Rais ameuza bandari, wewe sema mkataba huu haujakaa vizuri, utaeleweka, toa hoja kwa nini hauajakaa vizuri, upande wa pili watasema umekaa vizuri, lakini ukisema mkataba huu hata kichaa hawezi kuubali, maana nyingine unatuambia sisi sote ni vichaaa,” amesema.

Send this to a friend