Lugha ya Kiswahili imechaguliwa kuwa lugha rasmi kutumika katika mikutano yote itakayoendeshwa na Umoja wa Afrika (AU).
Akiongea na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku Umoja wa Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa nchi wanachama wa umoja huo zimekubaliana kutumia lugha ya Kiswahili kuendeshea mikutano yake yote.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika Kiswahili kama lugha halisi mojawapo ya kiafrika kimechaguliwa kuwa lugha rasmi itakayotumika katika mikutano yote ya Umoja wa Afrika ambapo siku za nyuma Kiswahili kilikuwa kinatumika kama lugha ya kazi na katika ngazi ya Mikutano ya Maraisi tu. Jambo hili ni la kujivunia kwa sisi Watanzania na Afrika kwa ujumla”, amesema Mulamula.
Balozi Mulamula pia ameongelea upande wa uchumi ambapo amesema mpaka sasa Afrika imepiga hatua kubwa kwani kuanzia Januari, mwaka huu nchi za Afrika zilianza rasmi kufanya biashara chini ya Mkataba ulioanzisha Eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA). Mpaka sasa nchi 54 kati ya 55 za Afrika zimesaini mkataba huo ikiwemo Tanzania, aidha, nchi 37 zimeridhia mkataba huo na Tanzania ipo kwenye hatua za mwisho za kuridhia mkataba huo.