Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ametoa maagizo kwa mahakimu kurahisisha masharti ya dhamana kwa Watanzania kujidhamini kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa (NIDA) katika mfumo wa haki jinai badala ya kutegemea watu wengine.
Ametoa kauli hiyo wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Tanga, na kuwataka mahakimu kuachana na mfumo wa makaratasi badala yake watumie mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha shughuli za utoaji haki kwa wananchi.
“Mtu anapojidhamini kwa kutumia kitambulisho cha Taifa anakuwa ameacha uraia wake mahakamani, hivyo hawezi kwenda popote bila kitambulisho hicho na kwamba inakuwa rahisi kumpata endapo atatoroka,” amesema Jaji Mkuu.
Maagizo mengine yaliyotolewa ni pamoja na mahakama kutokuwa wepesi kukubali hoja za waendesha mashtaka za upelelezi unaoendelea, pia alitaka mashauri ambayo washtakiwa wamekosa dhamana yasikilizwe haraka pamoja na kuwapo na matumizi ya adhabu mbadala.
Aidha amesisitiza mahakimu wahakikishe mahakama inakuwa sehemu salama kwa mtuhumiwa kwa kuwa ndio mahali pekee anayotarajia kupata haki kwa mujibu wa katiba.