Kituo cha daladala Mwenge kuanza kutumika Machi 2021

0
58

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge ameitaka Manispaa ya Kinondoni na mkandarasi kutoka JKT kuhakikisha ujenzi wa kituo cha daladala Mwenge na maduka 126 vinakamilika kabla ya February 28 na kuanza kutumika Machi Mosi 2021 ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Kunenge ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua miradi Wilaya ya Kinondoni ambapo amemuelekeza mkurugenzi wa manispaa hiyo kuhakikisha anampatia mkandarasi fedha kwa wakati ili mkandarasi asipate kikwazo cha kumfanya ashindwe kutekeleza agizo hilo.

Aidha, amewaelekeza wakurugenzi wa manispaa zote za jiji hilo kuhakikisha ifikapo Februari Mosi masoko yote yaliyokamilika yanaanza kutoa huduma kwakuwa lengo la ujenzi wa masoko ilikuwa ni kutumika na sio kubaki kama magofu jambo linalopelekea serikali kukosa mapato na wafanyabiashara kuendelea kubanana mitaani.

Akiawa kwenye ujenzi wa uwanja wa mpira wa KMC na maduka 79, RC Kunenge amewaelekeza JKT kuongeza kasi ya ujenzi na kusema kuwa anachokitaka ni kuona ifikapo Februari Mosi maduka yote 79 yanakuwa tayari yamekamilika na yamepata wapangaji.

Pia ametembelea Ujenzi wa Barabara za DMDP eneo la Bwawani na ujenzi wa Soko la Bwawani linalojengwa pia na DMDP na kuelekeza ifikapo Disemba 31 mwaka huu soko liwe limekamilika na mara baada ya kukamilika lianze kutumika ambapo amesisitiza Manispaa ya Kinondoni kuhakishisha wanaostahili kupata nafasi ya kufanya biashara wanapatiwa na kodi ya pango iwe nafuu.

Send this to a friend