Kituo kipya cha mabasi Mbezi Luis kuanza kutumia Novemba 30

0
58

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana amewatangazia wakazi wa jiji hilo na Watanzania kwa ujumla kujiandaa kutumia Kituo cha Mabasi cha Kimataifa cha Mbezi Luis kuanzia Novemba 30 mwaka huu.

Kuanza kutumika kwa kituo cha mabasi ya mikoani na nchi jirani hicho cha kisasa kutaweka ukomo wa matumizi ya kituo cha sasa cha Ubungo.

Wafanyabiashara wote wamekaribishwa kutuma maombi ya kupangishiwa maeneo ya kufanya biashara ambapo maombi yote yanatakiwa kutumwa kupitia www.pangisha.tamisemi.go.tz kuanzia Novemba 9 hadi Novemba 20 mwaka huu.

Aidha, wamachinga, mama na baba lishe wanatakiwa kiandika barua ya maombi na kuambatanisha na barua ya utambulisho kutoka kwa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa ili kupata ruhusa ya kufanya biashara kwenye kituo hicho.

Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 70 za Tanzania, utakapokamilika utakifanya kituo hicho kuwa moja ya kituo bora kati ya vituo vya mabasi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati huku kikitarajiwa kuchukua mabasi makubwa 108 kwa wakati mmoja.

Mbali na mabasi hayo, pia kitaweza kuchukua mabasi madogo zaidi ya mia moja huku kikiwa na huduma mbalimbali zikiwemo za migahawa, benki, zahanati kituo cha polisi, maduka pamoja na sehemu za kuoshea magari.

Kituo hicho kilitarajiwa kilitarajiwa kuanza kutumika Oktoba 2020 lakini mkandarasi alidai kushindwa kukamilisha ujenzi kutokana na janga la corona, na hivyo kuomba kuongezewa muda hadi Januari 2021.

Hata hivyo Rais Dkt. Magufuli alikataa ombi hilo na kuagiza kiwe kimekamilika kabla Novemba 30 mwaka huu.