KKKT pawaka moto, mchungaji agoma kuvuliwa Uaskofu

0
39

Askofu wa Dayosisi ya Konde, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Edward Mwaikali amegoma kuvuliwa uaskofu baada ya kiongozi Mkuu wa KKKT, Dkt. Fredrick Shoo kuitisha mkutano wa kumvua wadhifa wake.

Askofu huyo amedai kuwa mkutano ulioitishwa ulikuwa batili na hata wajumbe wa huo mkutano hawakuwa halali na utaratibu uliotumika haupo mahali popote pale kwa kuwa zipo taratibu za kikatiba  za kumuondoa Askofu lakini hazikuafuatwa.

“Mimi sikuhudhuria huo mkutano kwa sababu nilikuwa siutambui, na hili nilishasema tangu mwanzo nimesikia tu kwamba maamuzi ni hayo sijaambiwa rasmi, wakishaniambia nitakuwa na neno la kusema” amesema Mwaikali.

Anaendelea kusisitiza kuwa Mkuu wa KKKT amewatwisha laana wana Dayosisi ya Konde kwa sababu amekwepa kuwa mwenyekiti wa mkutano aliouitisha mwenyewe bila kushirikisha  Halmashauri Mkuu ya KKKT Konde, amenawa mikono kama alivyofanya Pilato.

Akitangaza matokeo hayo Dkt. Shoo amesema kati ya kura 211 zilizopigwa, kura 204 zilimkataa Dkt. Mwaikali huku kura tano pekee zikimkubali na kura mbili kuharibika.

Amesema baada ya hapo ulifanyika uchaguzi wa kumpata askofu mpya na kuchaguliwa Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu Mteule baada ya kupata kura 149.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Mbeya, Askofu Oscar Ongere amedai kuwa maamuzi ya Askofu Mkuu yamekuwa ya haraka na kuongeza kuwa jumuiya ilimtaka Askofu Shoo kusubiri kikao cha maaskofu KKKT nchini kitakachofanyika Jumatatu ili kupata maamuzi ya pamoja na kuondoa mvutano baina ya viongozi hao.

“Kwanza tuliunda tume huru ambayo ilibaini kuwepo kwa migogoro ya kikabila. Uamuzi huo wa Dkt. Shoo umekuwa wa haraka sana na hatujui ni kwanini, kuna mkutano wa maaskofu Machi 28 ambao ungetoa maamuzi,” amesema mwenyekiti.

Send this to a friend