Kodi za mabango na majengo zarudishwa halmashauri

0
44

Serikali imetoa muongozo mpya ambapo kuanzia sasa kodi za majengo, ushuru wa mabango na vitambulisho vya wajasiriamali vitasimamiwa na wakurugenzi wa halmashauri, tofauti na awali ambapo vilikuwa vikisimamiwa na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), lengo likiwa ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Wakitoa kauli ya pamoja kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Waziri Selemani Jafo amesema kuwa serikali imeamua kutoa madaraka kwa wakurugenzi wa halmashauri kusimamia vitengo hivyo kwa kuwa hao ndio wenye wigo mpana zaidi hadi ngazi za mitaa wa kufikia majengo yanayokusudiwa.

“Tumeamua kukubaliana wizara hizi mbili kuwa sasa mapato yote yakusanywe na wakurugenzi wa halmashauri ili wigo uwe mpana zaidi kodi za majengo yote zitakusanywa na Wakurugenzi na kuziingiza serikalini,” amesema Jafo.

Kuhusu ushuru wa mabango amesema wakurugenzi watakusanya ushuru wa mabango yote yaliyopo katika maeneo yao yaliyokuwa yakikusanywa na TRA, isipokuwa mabango yanayosimamiwa na Wakala za Barabara (TANROADS) na TARURA.

“Mabango yote yaliyokuwa yanasimamiwa na TRA sasa yote yatakuwa chini ya wakurugenzi, tunaamini ufanisi utaongezeka kwa kuwa wakurugenzi wanayajua mabango yote yaliyokatika maeneo yao kila aina ya bango na sehemu lilipo katika eneo hilo tunataka kuona ufanisi mkubwa wa ukusanyaji wa mapato” amesema.

Kuhusu vitambulisho vya wajasiriamali vilivyoboreshwa amesema tayari vimechapishwa na kupelekwa katika ofisi za TRA kote nchini na vitapatikana kwa bei ile ile ya shilingi elfu ishirini (20,000) kwa kitambulisho kimoja kitachomuwezesha kufanya biashara mwaka mzima.

Hata hivyo Mhe.Jafo amesema kuanzia sasa serikali haitarajii mfanyabiashara kufanya biashara bila kuwa na Cheti cha kulipa kodi ya TRA, leseni ya biashara ya Halmashauri au kitambulisho cha wajasiliamali, sheria kali zitachikuliwa kwa watu kama hao.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Hamis amewasisitiza wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi stahiki kwa Serikali ili iweze kujiendesha, na kuwataka wasimamizi katika kodi za majengo, mabango na vitambulisho vya wajasiriamali kusimamia kikamilifu.

Send this to a friend