Kontawa ajisalimisha jeshini, aomba kujiunga JKT

0
69

Msanii wa muziki nchini, Abdu Hamid Said maarufu ‘Kontawa’ amejisalimisha jeshini Lugalo jijini Dar es Salaam kurudisha mavazi yanayofanania na mavazi ya jeshi baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutaka mavazi hayo yasalimishwe.

Kontawa ambaye amekabidhi mavazi hayo mbele ya Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema kitendo cha kurudisha mavazi hayo ni kuunga mkono amri ambayo imetolewa na jeshi hilo huku akiliomba jeshi kumpa idhini ya kujiunga katika mafunzo ya kujitolea ya miezi sita kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambayo yametangazwa hivi karibuni.

“Ukiachana na chachu ya kuwa na nguo, na kuvaa nina hiyo ‘passion’ (shauku) ya kuwa kwenye sehemu kama hiyo, kwahiyo hili ni ombi langu kwenu kama itawezekana nipate miezi sita tu nirudi uraiani nikiwa nimenyooka,” ameomba Kontawa.

Harmonize: Wasanii kuweni na nyimbo za Kiingereza

Kanali Ilonda amempongeza Kontawa kwa kurudisha nguo hizo na kutoa wito kwa watu wengine kuiga mfano huo, huku akiwatoa hofu wananchi kutohofia juu ya usalama wao pindi watakapotaka kurudisha nguo hizo.

“Hatuna nia ya kukuuliza ulikuwa unaivaa wapi na wapi, hatutakuuliza uliipataje, hatutakuuliza unahifadhi wapi, sisi tunachukua mzigo na tukimaliza tutaagana, tutakusindikiza raha mustarehe ili mkaendelee kutekeleza majukumu yenu ya msingi,” amesema.

Send this to a friend